Rais wa Tanzania John Magufuli
ameliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ) kujenga ukuta
wa kuzunguka vitalu vya kuanzia A hadi D vyenye madini ya Tanzanite
katika eneo la Mererani, Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara ili
kudhibiti uchimbaji na biashara ya madini hayo.
Rais Magufuli alitoa agizo hilo
kwenye sherehe ya ufunguzi wa barabara ya Kia - Mererani iliyofanyika
katika eneo la Mererani.
Rais Magufuli amesema pamoja na
kujenga ukuta huo haraka iwezekanavyo, soko la Tanzanite litapaswa
kuwa katika eneo hilo, Tanzanite yote itapita kupitia lango moja na
ameitaka Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kushiriki katika ununuzi wa
Tanzanite.
"Lile eneo la kitalu kuanzia A
hadi D ambalo ndio lina mali nyingi ya Tanzanite, naagiza Jeshi la
Wananchi kupitia Suma-JKT na wengine, najua wameshamaliza utafiti,
waanze kujenga ukuta eneo hilo lote na kazi hii ifanyike haraka,
watakapojenga ukuta wataweka kamera na patakuwa na mlango mmoja
ambapo patajengwa vifaa maalum, nataka niwaeleze ukweli ndugu zangu
wa Simanjiro hata kama utameza Tanzanite itaonekana" amesema
Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli amevipongeza
vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zilizoanza kuchukuliwa
kukabiliana na wizi wa madini ya Tanzanite na ameitaka kamati
inayoongozwa na Waziri wa Sheria na Katiba Prof. Palamagamba John
Kabudi kuanza kufanyia kazi taarifa zilizotolewa na wananchi kuhusu
uchimbaji na biashara ya madini hayo ili mchakato wa kurekebisha
mikataba ufanyike.
"Ripoti ya kamati iliyoundwa
na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai
imeonesha kuwa Serikali na wananchi tunanufaika kwa asilimia 5 tu ya
madini haya ya Tanzanite, zinazobaki zote wananufaika watu wengine,
hii haiwezekani ni lazima tuwe na mikataba itakayotunufaisha na sisi,
haiwezekani Tanzanite tunayo sisi tu lakini tunapata asilimia 5,
halafu hapa Mererani hakuna maji na hakuna gari ya wagonjwa"
amesisitiza Rais Magufuli.
Hata hivyo Rais Magufuli amewaahidi
wananchi wa Mererani kuwa atawapelekea gari la wagonjwa na pia
atalifanyia kazi tatizo la uhaba wa maji linalowakabili wananchi hao.
Mapema akitoa taarifa ya ujenzi wa
barabara ya Kia - Mererani yenye urefu wa kilometa 26, Waziri wa
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa Mnyaa alisema
ujenzi huo umegharimu Shilingi Bilioni 32 na kwamba barabara hiyo
itaunganisha eneo la madini ya Tanzanite la Mererani na eneo la
uwekezaji la Mererani, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro
(KIA) na barabara kuu ya Moshi - Arusha.
No comments:
Post a Comment