Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
amemuagiza Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
“TAKUKURU”mkoa wa Mbeya, Emanuel Kiabo kumkamata na kumuhoji
aliyekuwa Meya wa Jiji la Mbeya Atanas Kapunga na wenzake 11 kwa
tuhuma za kuisababishia Serikali hasara ya sh. bilioni 63.448.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo
Jumatatu hii alipozungumza na watumishi wa Halmashauri za wilaya ya
Mbeya na Halmashauri ya Jiji la Mbeya katika mkutano uliofanyika
ukumbi wa Benjamin Mkapa.
“Serikali hii haiwezi ikawaacha
watu hawa ambao wameisababishia hasara kubwa kiasi hiki tena kwa
halmashauri moja. Kama wako humu ndani naagiza wakamatwe na waanze
kuhojiwa na ambao wamestaafu au kuhamishwa kituo cha kazi wasakwe
popote walipo ili nao waje kuhojiwa,” aliagiza Waziri Majaliwa.
Wengine ni waliowahi kuwa
wakurugenzi wa Jiji hilo ambao ni Bw. Mussa Zungiza, Bi. Elizabeth
Munuo, Bw. Juma Idd na Dkt. Samwel Lazaro aliyekuwa akikaimu nafasi
ya Ukurugenzi.
Aliyekuwa Mweka Hazina wa Jiji, Bw.
James Jorojik pamoja na waliokuwa wajumbe wa Bodi ya Zabuni ambao ni
Bw. Mussa Mapunda, Bw. Samweli Bubengwa, Bw. Davis Mbembela, Bi.
Lydia Herbert na Bw. Bernard Nsolo ambao walipitisha nyongeza ya
mradi huo bila ya kuzingatia maslahi ya Jiji pamoja Emily Maganga
ambaye hakuishauri vizuri bodi hiyo.
Waziri Mkuu amesema watumishi hao
wanatakiwa kuchukuliwa hatua stahiki za kisheria kwa kuwa
wameisababishia serikali hasara kubwa katika mradi wa ujenzi wa soko
la Mwanjelwa Jijini Mbeya ambalo hadi sasa halijaonyesha tija.
No comments:
Post a Comment