Kiongozi wa vyama vya muungano wa
upinzani nchini Kenya (NASA), Raila Odinga amewashauri wafuasi wake
kususia kazi kuanzia kesho jumatatu Agosti 14 kama njia ya kupinga
matokeo ya uchaguzi uliofanyika jumanne ya Agosti 8.
Akihutubia wafuasi wake huko Kibera jijini Nairobi kwa mara ya
kwanza tangu yatangazwe matokeo ya uchaguzi mkuu ambapo Rais Uhuru
Kenyatta alitangazwa mshindi, Bw Odinga amedai kuwa serikali ilikiwa
imepanga kuwaua wafuasi wa upinzani hata kabla ya matokeo kutangazwa.
Kauli hiyo inakuja baada ya watu 24 kuripotiwa kuuawa maeneo
tofauti ya jiji la Nairobi na Kisumu, wakati wafuasi wa upinzani
walipojitokeza kulalamikia matokeo ya uchaguzi.
Hata hivyo, Odinga amesema kuwa siku ya Jumanne, Muungano wa vyama
vya upinzani (NASA) utatangaza muelekeo wao kuhusu matokeo hayo ya
uchaguzi.
Katika kutafuta suluhisho aliyewahi kuwa katibu mkuu wa Umoja wa
mataifa, Kofi Annan, ambaye alikuwa mpatanishi mkuu baada ya mzozo wa
kisiasa nchini Kenya miaka kumi iliyopita, ametoa wito kwa Bw Odinga
kutumia mifumo ya kisheria kutafuta haki kuhusu matokeo ya uchaguzi
wa urais.
No comments:
Post a Comment