
RAIS John Magufuli amekazia msimamo wake wa kutaka kujua
kila kilichomo kwenye makontena ya mchanga wa dhahabu baada ya kuwataka wajumbe
wa kamati maalumu aliyounda kutumia utaalamu wao wote katika kupata ukweli bila
kuyumbishwa na mtu.
Rais Magufuli (JPM) alitoa maelekezo hayo Ikulu jijini Dar
es Salaam, jana, wakati akiwaapisha wajumbe hao wa kamati maalumu aliyounda
kuchunguza kiwango na aina ya madini yaliyomo kwenye mchanga wenye madini ulio
ndani ya makontena yaliyoko katika maeneo mbalimbali nchini.
Taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais
Ikulu, ilieleza kuwa hafla ya kiapo kwa wajumbe wa kamati hiyo ilihudhuriwa na
viongozi mbalimbali wakiwamo Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju;
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi; Kamishna wa
Maadili, Jaji Harold Nsekela na viongozi wa vyombo vya ulinzi na usalama.
Taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa Rais alitoa maelekezo hayo
baada ya kuwaapisha, akisema kuwa ameamua kuunda kamati hiyo yenye wasomi
waliobobea katika masuala ya jiolojia, kemikali na uchambuzi wa kisayansi ili
wawawakilishe Watanzania zaidi ya Milioni 50 ambao wanataka kujua ukweli kuhusu
rasilimali yao ya madini.
“Hivi sasa duniani kuna vita nyingi na vita mojawapo ni vita
ya uchumi, kwa hiyo tunawatuma nyinyi mwende mkapigane vita hii katika sekta
hii ya madini, mkawawakilishe Watanzania zaidi ya Milioni 50, mkapate ukweli
wote na wala msikubali kuyumbishwa na mtu yeyote,” alisema Rais Magufuli na
kuongeza:
“Tumieni utaalamu wenu, busara zenu, uzalendo wenu kwa Taifa
na upendo wenu kwa Watanzania hasa masikini wenye shida nyingi.”
Kamati hiyo ya wanasayansi wanane iliteuliwa na Rais
Magufuli Machi 29 na inaongozwa na Mwenyekiti wake Prof. Abdulkarim Hamis
Mruma. Itafanya kazi ya uchunguzi kwa siku 20 kabla kuwasilisha ripoti yake kwa
Rais.
Aidha, Rais Magufuli aliwahakikishia wajumbe wa kamati hiyo
kuwa Serikali itatoa kila aina ya ushirikiano kwao ili kufanikisha kazi hiyo na
ametaka wawe huru kutumia vitendea kazi vyovyote vinavyohitajika, ikiwamo maabara
mbalimbali za taasisi za Serikali na nyinginezo.
“Nendeni popote mnapohitaji kufanya kazi tutawapa
ushirikiano, fungueni makontena popote yalipo, chukueni sampuli na mkazipime
mjue kilichomo na naviagiza vyombo vya dola vihakikishe hakuna mtu atakayewakwamisha,”
alisema Rais Magufuli.
WACHUMI, WANASHERIA PIA KUCHUNGUZA
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alisema baada ya kuunda
kamati hiyo ya wanasayansi, ataunda kamati nyingine ya wachumi na wanasheria
kwa ajili ya kufanya tathmini na kuiangalia sera na sheria ya madini kwa lengo
la kupata taarifa zaidi juu ya biashara ya madini hapa nchini.
Hivi karibuni, Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza
katika bandari ya Dar es Salaam na kukuta makontena 20 ya mchanga wa dhahabu
yaliyokuwa tayari kusafirishwa kwenda nje ya nchi.
Siku chache baadaye, yalibainika makontena mengine 262 yenye
mchanga wa dhahabu yakiwa yamehifadhiwa baada ya kufuata taratibu zote za
kuyasafirisha kwenda nje.
Uongozi wa Mgodi wa Acacia wenye sehemu kubwa ya makontena
hayo yaliyoko bandarini Dar es Salaam ulitoa ufafanuzi kuwa makontena hayo
yalifikishwa baada ya mchakato wake kufanyika kabla ya agizo la Rais kuzuia
usafirishaji wa mchanga aina hiyo kwenda nje ya nchi.
KIONGOZI WA KIHINDU
Wakati huo huo, Rais Magufuli alikutana na kufanya
mazungumzo na Kiongozi Mkuu wa Jumuiya ya Kihindu ya BAPS Swaminarayan Sanstha
Duniani, Mtukufu Mahant Swami Maharaj ambaye yupo nchini kwa ziara ya siku 7.
Pamoja na kumshukuru kwa ujio wake nchini, Rais Magufuli
alimhakikishia kuwa Serikali ya Tanzania itaendeleza na kuimarisha zaidi
uhusiano na ushirikiano wake na Jumuiya hiyo na amewaalika wafanyabiashara
walio chini ya Jumuiya hiyo kuja nchini Tanzania kuwekeza katika viwanda,
kilimo na shughuli nyingine za biashara na uwekezaji.
No comments:
Post a Comment